Ubora unaonekana kwa kile unachokifanya kila siku na si kwa kile unachokifikiria pasipo kukifanya.
Kile unachokifanya sasa hata kwa kiwango cha chini sana, ukiwa na nia ya kukua zaidi itakuwa hivyo.
Changamoto unazokutana nazo kwa kile unachofanya, zinakuimarisha zaidi kuwa bora kuliko ungekuwa unaongea na kufikiri tu pasipo vitendo.
Unayemwona yupo vizuri leo na amekuzidi vitu fulani, hakuanza hivyo.
Unachokiona kizuri sana na kinakuvutia, hakikuanza hivyo.
Kukosea ni hatua ya kuelekea kile unakitamani.
Usifikiri kile unachokitamani kiwe kwako, kitatokea tu siku moja ukiwa umelala/umekaa la hasha lazima uanze hatua kwa hatua.
Unatamani kuwa mwandishi mzuri anza na maneno hamsini tu kila siku, haijalishi unakosea ama unajikisia uvivu.
Utamani kuwa msomaji wa biblia/vitabu anza na ukurasa mmoja tu kila siku.
Unatamani usiwe na tabia ya kuropoka ropoka ovyo maneno yasiyo na msaada kwa watu, anza kukaa kimya ilazimishe akili yako kutaka kujifunza kwa wenzako.
Chochote unachokitamani anza hatua moja kuelekea hatua ya pili, haijalishi utakosea, huko ndio kujifunza kwenyewe na hutokosea hilo eneo tena maana tayari unajua namna ya kuepuka.
Ifike wakati watu wajiulize ulibobea wapi huo ujuzi ulionao sasa ili iwe chachu kwao kujifunza.
Kabla hujaondolewa huu uhai, unapaswa kuandikwa kwenye historia ya vitabu kuwa huyu mtu alikuwa mwanzilishi wa hichi kitu.
Ifike muda miongoni mwa njia ulizopitia watu watamani kuzijua kwa nia ya kujifunza kuwa bora.
Ifike muda hata kama hutokuwepo hapa duniani, watu watumie maneno/sauti yako kujifunzia.
Ukikaa na kuendelea kusubiri itokee kwa miujiza hicho utachosikia msukumo ndani yako kukifanya, unaweza usione kikitokea mpaka pale utakapoamua kuchukua hatua.
Ubora wa hao unaowapenda na kutamani kuwa kama wao, walianza kwa kuchekwa na kukatishwa tamaa, ila wao walitazama kusudi lao... kelele na maneno ya kuvunja mioyo yao walichukulia kama darasa kwao.
Amua kuendelea kuongea pasipo kuchukua hatua yeyote ama amua kutenda.
Ndg Samson Ernest.
+255759808081.
0 maoni:
Post a Comment