Mwanamke Akiwa Anafanya Vitu Kwa Kujiamini Mbele za watu Ujue...

Habari za leo ndugu msomaji wa Mtazamo Wa Maisha, bila shaka unaendelea na maandalizi ya kumchagua rais wa nchi yako, na mbunge na diwani, nikushauri kwamba kelele zisikuchanganye ukakosa mwelekeo na usiende kwa hisia sana ukapoteza haki yako, nenda kwa hoja, na uwe na kadi ya mpiga kura, ukumbuke pia baada ya uchaguzi kuna maisha. Nikiwa nimeanza na salamu za kisiasa, usianze kufikiri huyu mwandishi yeye labda yupo chama gani mbona ameanza hivi, mimi sina chama ila nina kadi ya mpiga kura, na siku ya kupiga kura nitaenda kwa uaminifu kabisa, nami nimeamua kukushirikisha hili usipoteze haki yako ya msingi, tunaomba Mungu atupe kiongozi bora ila vitendo pia vinahitajika ambapo ni wewe na mimi kwenda kupiga kura.

Baada ya kumaliza kuwekana sawa hapo juu, nikualike kwenye makala hii ya kujua ufanye nini kumsaidia mwenzako ambaye upo naye ndani kufikia malengo yake kwa ujasiri pasipo kukatishwa tamaa na watu wa nje, siku zote tunajua ndoa ya mke na mume ni kushikamana kwa yale maeneo ambayo mwenzako alikuwa anapelea na wewe unaenda kuwa msaada kwake, ikitokea mmoja wapo amelegea kwenye eneo lake, upande mmoja huwa dhaifu na huo udhaifu hupelekea kupunguza ufanisi wa kazi na hupoteza ujasiri wa kujiamini mbele za watu pale anapofanya jambo, hii mara nyingi hutokea kwa wote kati ya mwanamke/mwanaume kutokana tu na jinsi mwenzake atavyomchukulia, nikutolee mfano kwa mwanaume ambaye ndoa yake ina shida na mke wake hampi ushirikiano kwa kile anachofanya nakwambia kama ni boss wako kazini uwe makini sana maana miongoni mwa vitu vinavyosababisha wafanyakazi wengi kufukuzwa kazi ni wakati mwanaume yupo kwenye kipindi kigumu kwenye ndoa yake.
Sasa Mimi leo nizungumzie mwanamke anapokuwa hana mwongozo mzuri kwa mmeo, tuelewe kwamba mwanamke ni chombo cha tofauti sana na kina nguvu kubwa sana pale kinapopewa nafasi ya kufanya jambo kwa ufanisi, sifa nyingine ya mwanamke ni mtu anayeweza kuhifadhi vitu vingi kwa wakati mmoja na akafanyia kazi kwa asilimia fulani tofauti na mwanaume anaweza kuwa anaongea na simu tu akashindwa kufanya kitu kingine kwa ufanisi, wakati mwanamke anaweza akafanya hivyo vyote, anaongea na simu huku anaendelea kuandika ujumbe ambao unaenda sehemu ukasomwa na watu wakaelewa, anaweza kupika wakati huo analea mtoto wakati huohuo anaosha vyombo wakati huo ameweka airphone masikioni anafuatilia kitu fulani kwenye  radio/audio. Mwanaume Unaweza ukastajaabu haya na unaweza ukasema naongea uongo, nikuombe radhi na unisamehe kwa kunifikiri hivyo ila nikupe kazi moja tu mwanaume kati ya hayo niliyosema na mengine ambayo sijataja naomba umfuatilie mkeo ama mwanamke yeyote unayeona anajitambua vizuri kwanini awe anajitambua, asilimia kubwa wasiojitambua wana ka uvivu fulani kabaya anaweza akakukera kabla hujamaliza zoezi lako. Kingine kama una jambo unahitaji kulitimiza tarehe fulani unajua kabisa kuna hatari ya kusahau usipokumbushwa mweleze vizuri na umwambie na lina uzito gani na madhara gani pale usipolifanya uone kitatokea nini ikifika hiyo siku, nikusaidie kwamba atakukumbusha mapema sana kabla ya siku husika.

Huyuhuyu mwanamke akikosa msaidizi wa kumsaidia na kumshauri kwa kile anachokifanya, atakuwa ana haribu sana maeneo mengi tofauti na mwanaume anaweza akawa ana shida hiyo ndani na akaendelea kuwa vizuri tu, kama mwanaume atakuwa mtu wa kumkosoa mke wake mbele za wageni/watoto kuwa hajapika vizuri badala ya kusubiri waondoke alafu mkiwa wawili unamwambia aisee mke wangu leo ulichemka kupika mboga, yaan umejaza maji na chumvi, wali wa leo kwa kweli una kiini, baada ya kumweleza hivyo atakueleza sababu iliyomfanya apike hivyo ama yaweza kuwa sio yeye aliyepika akiwa ni yeye utamwelekeza kwa upole ukiwa na wewe kesho unakuwa wa kwanza jikoni, utasema hapa sasa unatuzalilisha wanaume, la hasha! lazima kile usichokipenda kwa mwenzako uwe mfano namba moja kuonyesha kutopenda kwa vitendo vya kumsaidia mwenzako.

Ukiona mwanamke yupo mbele za watu anaongea kwa kujiamini sana alafu mme wake yupo mahali pale ujue jamaa yupo kwenye eneo lake la kuwajibika, lakini ukiona mwanamke anaongea kwa kujishtukiashtukia na ana hofu nyingi za kujihisi anakosea kwa kuona watu wanacheka ujue ndani kuna shida kubwa sana.
Ufanye nini sasa kuepukana na hili janga? kwanza jua kabisa mwanamke akishakupenda ni rahisi sana kukopi kila kitu unachofanya, ukiwa unajiamini sana na yeye anajiamini, ukiwa mvivu sana na yeye akianza kufanya jambo anakukumbuka, kufanya hivyo anaacha kufanya kwa moyo, ukiwa mwongo kuna vitu ataacha kukushirikisha, ukiwa mkorofi kwake hapo ndio unasababisha afanye vitu vingi sana kwa siri, usishangae kusikia amejenga nyumba yake sehemu na sasa ni mwaka wa pili/tano anapangisha na kodi anakula.

Mwanamke sio chombo kidhaifu kama unavyofikiri wewe, unaweza kuwa hujui udhaifu unaosemwa, kuna uwezekano mkubwa sana hukumwelewa aliyesema hivyo, kama ni hivyo kwanini wanatumiwa kwenye maeneo nyeti kuwapeleleza wanaume watoe siri zao za maisha yao? kwanini wewe mwanaume usiitwe dhaifu? Acha ukoloni, hatupo tena utumwani, usiwe kama rafiki yangu mmoja nilikuwa naye mwezi ulioisha juzi akawa anaongea na simu kwa maneno makali sana, nilimwacha amalize kisha nikamuulize hivi unaongea na binti wa watu vibaya hivyo unafikiri ndio atakuheshimu? kwanini nilijua moja kwa moja ni mwanamke ni mazungumzo yake tu ,naamini mwanaume hawezi kuongea na mwanaume mwenzake vibaya hivyo labda wawe wanadaiana pesa, alichonijibu ni kwamba yaani wewe ndugu yangu usipokuwa makini utaendeshwa/utapelekeshwa sana na mke wako! Moja kwa moja nikajua malezi na mazingira yamemharibu saikolojia yake amejua mwanamke yeye ni mtu wa kusemeshwa kwa sauti kali na ya vitisho ndipo anakuwa na hofu kwa mmeo.

Nimalize kwa kusema kwamba ondoa mitazamo hasi, na kuwa na mitazamo chanya, ondoa historia ya maisha yako uliyoishi hapo nyuma ukiona watu wanavyowapelekesha wenzao katika ndoa, jua mnapokuwa wanandoa nyie ni marafiki mlioshibana haswa ndio maana mkaoana, mkikosana msameheane na sio mchukiane, maana huyo sio mchumba mkikorofishana tu mwaweza achana, huyo ni mkeo mwonye kwa upole, akishupaza shingo ndio ukaze sauti sasa, mtie moyo kwa kila jambo analofanya vizuri, anakutunzia watoto wenu mtie moyo kwa kumfanyia vile vitu ambavyo unajua kabisa hapa nikifanya hivi atafurahia tu maana wewe mwenyewe unalifurahia, akiwa na huzuni uwe mfariji wake kwa muda huo, usiwe na wewe unamwelezea shida zako ulizokutana nazo huko nje, joto lako kwake ni la mhimu sana sio kwa watoto wako tu.

Nikushukuru sana kwa kuwa pamoja nami, pia nikushukuru kwa kunipa muda wako, naamini umejifunza jambo jipya la kujenga mahusiano yako ya ndoa, kama bado hujafikia ndoa na upo katika mahusiano ya uchumba nikuombe usiwe kero kwa mwenzako, usimuumize kichwa sana mwenzako nakwambia atakukimbia. Ishini kwa upendo mkiilinda sana amani yenu isiondoke katikati yenu.

Ni mimi Rafiki yako Samson Ernest, usiache kutembelea mtandao huu kwa mambo mazuri zaidi.

samsonaron0@gmail.com
WhatsApp 0759808081.

SHARE

Samson Ernest

Habari, mimi ni mwandishi na mhamasishaji ambaye ninapenda kuona maisha ya kila mtu yakiwa bora. Naamini kila mmoja wetu anaweza kuwa na maisha mazuri kama ataamua hivyo. Karibu ujifunze kupitia mtandao huu wa MTAZAMO WA MAISHA.

  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

Post a Comment