Madhara Ya Kucheka Ovyo Na Jinsi Ya Kuepuka Kucheka Ovyo.

Kuamka ni hiari, kufanya ni hiari, kuchagua ni kuamua wewe, na kusoma hapa ni wewe kuamua usome ama upite kwanza uwahi kuchati na rafiki yako, habari za leo rafiki wa mtandao huu wa MTAZAMO WA MAISHA ,furaha yangu ni wewe kuamka na kuweza kufungua hapa na kusoma makala hii, hata kama kuna jambo linakuumiza kichwa ama unajisikia kuumwa isiwe sababu ya wewe kusinyaa moyo bali jua una bahati ya pekee kuiona leo.
Baada ya salamu na maneno machache ya kukumbushana umhimu wa wewe kuona siku mpya, tuje kwenye somo letu, mara nyingi furaha/amani/upendo ndani ya moyo wa mtu huwezi kuizuia kwa kumwambia asicheke pale anapofurahishwa na jambo fulani ndani ya moyo wake.
Kuna watu wanamaliza miezi hajawahi kucheka, wala kutabasamu, hii inaweza kutokana na mazingira ya kazi yake vilevile inaweza ikatokana na mambo yanayomsibu ndani ya maisha yake, anajikuta amekata tamaa mpaka hata ile ladha ya kucheka inakosekana kabisa.

Unaweza ukawa na furaha nyingi sana ukashindwa kujizuia lakini jua hiyo furaha ina sehemu zake za kuitoa, sio kila muda unaweza kucheka kila mahali, itashangaza watu wapo kwenye msiba alafu wewe unaangua kicheko, inashangaza mtu amesimama mbele ya halaiki kuongea vitu visivyo vya utani wewe unaanza kucheka, inashangaza upo eneo ambalo kila mtu yupo bize na mambo yake na ameelekeza umakini kwenye eneo lake wewe una mwangalia unaanza kucheka, hii tabia unaweza ukaona ni ya kawaida kabisa kwako ila ni mbaya sana kwa watu wanaokuzunguka, kwanini nasema hivi? ifike wakati watu wajue hili limekufurahisha na hili halijakufurahisha, kama limekufurahisha sio lazima ucheke sana mbele ya halaiki wakati unaona wenzako wapo kwenye umakini mkubwa wa kusikiliza kile wanakipata sasa kama wewe utacheka katikati ya kundi hilo na msemaji hajachekesha utaonekana akili zako hazipo sawa, au haupo makini, au una dharau, au hujielewi.
Kucheka ovyo mara nyingi huambatana na utani usio na kipimo, wakati wenzako wapo siriaz wewe unacheka na kutoa maneno ambayo hayahusiani na mada husika, ukija kushtuka kuwa ulichokuwa unafanya si sahihi tayari utakuwa umejenga picha mbaya kwa wenzako, watakuwa wanakuona ni mtu asiyekuwa na umakini wa mambo, unaweza ukaongea kitu chenye maana ila wakakipuuzia kutokana na wewe ulivyo.

Ieleweke kwamba kila jambo/kitu ni kizuri kama kitatumika sehemu yake sahihi, mfano; simu ni nzuri sana kwa matumizi na hakuna asiyejua umhimu wa simu, na hakuna mtu anayeweza kuona kero kwa simu yako kuita ila pale mnapokuwa sehemu yenye kuhitaji uzime simu alafu hukuzima ikaita kwa sauti utaonekana una dharau/haupo makini, Friji lako ni nzuri sana ila huwezi kwenda kuweka nguo zako, viatu vyako ni vizuri sana ila huwezi kuviweka kitandani, zingatia sana hili na uelewe kwamba kila kitu unachokiona hapa dunia kina eneo lake la kufiti.

Ufanyaje sasa kuepukana na hali hii ya kujikuta umecheka ovyo pasipo kutegemea? kwanza kabisa jua shida yako inakuwa wapi, kisha ifanyie kazi, shida ipi sasa? kwa kuwa rafiki yako nipo hapa naweza kukusaidia kujua namna ya kufanya, unaweza ukajiuliza sasa mimi nitajuaje shida yangu wakati mimi nina furaha na lazima nicheke, hujakosea kabisa ila ni kwamba unacheka hata sehemu ambazo si za kucheka, hii inatokana na kutoweka akili yako eneo husika, mfano mimi naandika makala hii kuna uwezakano labda nikawa nachati na mtu mwingine yaani naingia na kutoka, naweza nisifikishe ujumbe tarajiwa kwa wakati na naweza nisifikishe ujumbe inavyopaswa kumfikia mtu kwa sababu sijaweka nguvu yangu ya akili sehemu moja, sasa wewe unaweza kuwa mpo sehemu ya kusanyiko la watu mnasikiliza hotuba/semina fulani wakati huohuo unachati na simu sasa ile kuchati unajikuta unacheka kwa nguvu mpaka watu wote wanakuangalia wewe au wakati mtoa mada yupo mbele wewe unakuwa unamlinganisha na mtu mwingine ambaye huwa anakuchekesha, ama aliye mbele yako huwa ni mtu wa vichekesho japo muda huo hachekeshi zaidi anaongea vitu vya msingi na watu wamejenga utulivu kwake.
Unapojikuta kwenye hali hii ya kucheka pasipo mpangilio wowote, jijengee nidhamu binafsi kama unavyofanya kujitengenezea nidhamu za mtumizi ya pesa/muda hata eneo hili pia unaweza ukafanya  hivyo, ukiwa kwenye eneo lolote lile, soma mazingira yanahitaji nini, uwe na furaha, tabasamu, kuhuzunika, kuongea sana, au kukaa kimya sana hii ni mhimu sana, ukijua hili itakusaidia sana. Kingine tengeneza umakini wa kupokea kitu kipya kwa mzungumzaji aliye mbele yako, hii pia itakufanya uwe na nidhamu kubwa sana, nikufikirishe, hivi umewahi kujiuliza kwa nini watu ambao huwa hawacheki/kuongea ovyo ovyo wanaogopwa sana si kana kwamba wao ni watu wa tofauti ila jinsi walivyojiweka ndio wanaonekana hivyo sasa wewe sikufundishi kununa/kukunja ndita bali nakufundisha kuitumia furaha yako vizuri usionekane kero kwa wengine.

Zingatia sana haya, jua wewe ni mtu wa maana sana unahitaji kutoa msaada kwa wengine ila utashindwa kama kila eneo wewe utacheka tu ovyo kwanza watakudharau alafu utaanza kulalamika mbona watu hawanisikilizi, vivyo hivyo kwenye kuonyesha uso usio taka masihara pawepo na sehemu na muda wake iwe kazini/nyumbani kwako lazima wafanyakazi/familia yako itambue hapa leo tumemkwaza huyu kwa kufanya hili sio kila saa wewe ni mkalimkali tu. Nakwambia watakuzoea na kukuona wa kawaida tu hata ukiwa unaongea kwa ukali na kuonyesha hutaki masihara watakuona ni yule yule tu wajana. Nimalize kwa kusema kwamba badilika kutokana na mazingira, angalia mazingira yanahitaji nini kutoka kwako kwa muda huo.

Rafiki yako  Samson Ernest  waweza kunipata facebook kwa  jina hilo hilo.
Kwa mawasiliano zaidi piga 0759808081/0715591559.

SHARE

Samson Ernest

Habari, mimi ni mwandishi na mhamasishaji ambaye ninapenda kuona maisha ya kila mtu yakiwa bora. Naamini kila mmoja wetu anaweza kuwa na maisha mazuri kama ataamua hivyo. Karibu ujifunze kupitia mtandao huu wa MTAZAMO WA MAISHA.

  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

Post a Comment