Unamwona Mke/Mume Wako Wa Ndoa Hakufai Tena? Jibu Lako Lipo Hapa.

Habari za siku mpenzi msomaji wa makala za MTAZAMO WA MAISHA. Matumaini yangu unaendelea vyema, na kama haupo vizuri kiafya nikupe pole sana, Mungu akupe uzima ili uendelee kuleta mabadiliko ya maisha yako.
Nikualike katika makala ya leo, inayozungumzia mahusiano ya ndoa. Inaweza kuwa umefika wakati huna tena hamasa ya kuonyesha upendo wako kwa mkeo/mumeo.

Umefika wakati huna tena ile hamu ya kuendelea kumwona mke/mume wako. Kila ukifikiria huyu ni mume/mke wangu unakosa furaha kabisa, si kana kwamba unafanya hivyo kwa kupenda wala si kana kwamba unapenda iwe hivyo ila imetokea unamchukia tu mkeo/mumeo.
Kila anachokifanya mumeo/mkeo unakiona ni upuuzi fulani hivi kwako, mke/mumeo anaweza kuwa anakuongelesha jambo fulani hivi zuri la kuhitaji msaada wako wa mawazo. Ila ndani mwako hujisikii kabisa kutoa chochote cha kumshauri.

Upo tayari kuongea masaa mengi na mume/mke asiye wako, ila kwa mkeo hata dakika tano tu unaona kama masaa sita. Imefika wakati sasa umeanza kufikiri, hivi Mungu nilikosea wapi kuoa/kuolewa? Mbona hii ndoa imekuwa ndoano?.
Ukiwa una uhakika ndani ya moyo wako, kabla ya kuoa/kuolewa na huyo mumeo/mkeo hukulazimishwa na mtu yeyote, wala hukumwona ana kasoro yeyote. Na mpaka inafika siku ya kuoa/kuolewa una amani kabisa ndani ya moyo wako, na siku hiyo ulisherekea kwa amani. Ni ishara kwamba ulimpenda mwenzako.

Jiulize, iweje leo hii umeanza kumwona mwenzako hakufai, iweje leo hii umeanza kuona wadada/wakaka wengine wazuri. Na unataka utembee nao ama unatamani dada/kaka fulani angekuwa mumeo/mkeo. Umejitahidi kufanya kila mbinu angalau lile pendo lako la mwanzo lirudi, lakini hakuna chochote.

Unajiuliza ufanyaje sasa? jibu sio kuachana na  mkeo/mumeo, wala jibu sio kwenda kwa waganga wa kienyeji kutafuta limbwata la kumfanya mkeo/mumeo akupende tena, Na akusikilize kuliko mtu mwingine, wala msiba wako sio wa kukimbilia kwa kila MTUMISHI WA MUNGU kuombewa. Sawa sio mbaya ila kuna uwezekano mkubwa hapo ulipo umefanya hivyo sana ila huoni matokeo yeyote.
Umewaita ndugu/jamaa/marafiki/wazazi/mashemeji wakusaidie kurudisha amani ya ndoa yenu. Lakini cha kushangaza wanaongea weee, mnakubaliana hiyo hali haitarudia tena. Wanatoka tu siku mbili tatu, wanasikia yamerudia yale yale tena.

Nakuomba ufanye jambo hili; Usimlaumu mke/mume wako kwa leo, kama wewe ndio huoni tena ule uzuri wa mkeo/mumeo. Tulia usiwe na hofu, na kama mkeo/mumeo hakuoni tena una umhimu kwake tulia upate mwongozo.

1. Mke wangu sitaki hata kumwona; Kama wewe mwanaume unapitia hali hii, nakuomba ufanye hichi kitu. Anza kukumbuka ile siku ya kwanza kabisa wakati unakutana na mke wako, ambapo wakati huo mlikuwa wachumba. Nenda taratibu, kumbuka siku unamtamkia unampenda, kumbuka siku unamwambia hakuna mwanamke mwingine mzuri kama wewe, kumbuka siku unahangaika usiku na mchana akukubali kuwa mume wake, kumbuka ule uzuri wake uliokufanya ukose amani pale anapokosekana hewani, kumbuka ile siku uliyomsubiria kwenye giza maana wakati huo hakukuwa na simu za kupigiana kama sasa hivi.
Endelea na hili zoezi taratibu, ikiwezekana uwe sehemu ya peke yako kabisa, zima simu zako, usiwe kwenye makelele.

2. Mume wangu sitaki hata aniguse; mwanaume amekuwa kama vile mzigo kwako? ndio amekuumiza kwa mambo mengi, je we unajua kabisa umecheza eneo lako kama mke vizuri? na wewe jenga utulivu. Kumbuka siku zile huambiliki wala husikii kuhusu handsome wako, kumbuka zile siku usipoambiwa neno NAKUPENDA unajisikia kama vile umenyimwa haki yako ya msingi kabisa.
Nenda taratibu, siku unahangaika usiku na mchana kumtetea mwenzako kwa marafiki/wazazi wako kuwa ni mwanaume makini na mwenye roho ya utu, kumbuka zile siku hata mkilala njaa huoni shida. Unajua kesho tutapata, kumbuka zile siku mlikaa muda mrefu bila mtoto. Lakini mlipendana sana, mawifi walikucheka na kukutukana, lakini ulivumilia yote, na hii una watoto.

Baada ya kila mmoja wenu kufanya hili zoezi, umejisikia nini ndani ya moyo wako? nina imani kuna kitu kimeanza kukusukuma ndani yako, nina imani kuna nguvu ya upendo imeanza kukusisimua ndani yako, nina imani unajisikia kumwomba msamaha mwenzako.
Kama ni mwanamke, fanya hivi; pika chakula kile ambacho unajua mumeo anakipenda sana, kama una dada wa kazi mwambie leo pumzika.
Onyesha ujuzi wako, pika chakula kilichoenda darasani. Andaa mezani mkiwa na mumeo tu, katikati ya chakula anza kuonyesha machozi ya majuto kwa ulichomfanyia mumeo. Omba msamaha ukimaanisha, alafu mkumbushe mumeo jambo moja tu mlilowahi kuahidiana.

Na wewe mwanaume, fanya hichi; tafuta jioni moja tulivu. Nenda na mke wako sehemu nzuri yenye madhari iliyotulia, siku hii mke wako asipike wala asitembee kwa mguu,, uwe una gari au hauna, kama mnaenda hiyo sehemu asitembee kwa mguu. Tafuta hata usafiri wa kulipia, nunua zawadi ambayo unajua kabisa hapa mke wangu atajua leo mume wangu amerukwa na akili au namfananisha.
Wakati mmetulia na mnaendelea kula, anza kuongea kwa sauti ya upole sana. Mwite lile jina ambalo hapo nyuma alikuwa akilisikia tu, yeye hoi.
Mwambie mke wangu sijapendezwa na haya maisha ya kukosa amani, omba msamaha. Kisha mtolee ile zawadi uliyomnunulia, akiipokea, usisite kumkumbatia kwa furaha kubwa.

Mpaka hapo ndoa yako imepona, usirudie tena makosa, endeleeni kufurahia ndoa yenu.
Usisite kuniandikia ujumbe au kunipigia simu kwenye no 0759808081, kunijulisha matokeo.
Usiache kutembelea mtandao huu wa MTAZAMO WA MAISHA kwa makala zingine nzuri zaidi.

Rafiki yako Samson Ernest.

SHARE

Samson Ernest

Habari, mimi ni mwandishi na mhamasishaji ambaye ninapenda kuona maisha ya kila mtu yakiwa bora. Naamini kila mmoja wetu anaweza kuwa na maisha mazuri kama ataamua hivyo. Karibu ujifunze kupitia mtandao huu wa MTAZAMO WA MAISHA.

  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

Post a Comment