Huyo Ni Mke Wako Na Si Wawazazi/Ndugu zako.

Habari za wikiendi rafiki yangu, matumaini yangu unaendelea vyema, na kama u mgonjwa nikupe pole. Vizuri pia ukaenda kuangalia unasumbuliwa na nini kama ulikuwa bado hujaenda kumwona daktari.

Tukumbushane kwamba, mwanaume unapoamua kuoa haupaswi kufikiri kwamba kuoa mke ni kwa ajili ya kusaidia kazi ya nyumbani tu, jua kwamba huoi dada wa kazi, wala huoi ili kuwafurahisha wazazi wako tu, ni zaidi ya hilo.

Elewa kwamba Mungu sio kana kwamba hakujua alivyosema atamwacha baba na mama yake, ataambatana na mme wake.
Hajasema ataambatana na wazazi wa mume wake wala ndugu zake na mume wake.

Tabia ya kuoa mke alafu unaenda chumba cha pili, cha wazazi wako, choo kimoja, bafu moja, bomba/karo la maji moja, beseni/ndoo za kufilia na kuogea moja, jiko la kupikia moja... Ni kosa baya sana, ambalo wanaume wengi hufanya.

Mwanamke hawezi kuwa huru katika kufikiri familia yenu itakuwaje miaka miwili, mitatu, minne ijayo... kama utamweka nyumba moja na wazazi wako. Kumbuka aliona muda wa kuishi na wazazi umeisha, na akaona vyema asipoteze muda bali awe na mwenza wake.

Ina maana wewe mwanaume faida yako, ya kuoa mke ni kwa ajili ya tendo la ndoa tu? haiwezekani mtoto wa watu afanye kila kazi ya ambayo kwao hakuziweza kuzimaliza.

Haiwezakeni mke wako amekuwa mfanyakazi wa dada/kaka zako ama wadogo zako, kwa kuwa hawezi kukuambia ama hawezi kusema, ama akisema unakuwa mkali. Pia hataweza kukaa amejikunyata mikono hata kama amechoka, ikiwa anaona mama yako anafua nguo za baba yako.

Hataweza kuendelea na shughuli zake, za kuleta maendeleo ya nyumba yenu na watoto wenu, pale anapoona anahitajika kujumuika na shughuli za nyumbani.

Unakuta nyumbani hakuna bomba la maji na kama lipo halitoi maji, mke wako anafanya kazi ya kusomba maji ya nyumba nzima, na kama tujuavyo familia nyingi za namna hii hazikosi kuwa na idadi kubwa ya mawifi na mashemeji.

Sasa huyu dada/mama atafurahia lini ndoa yake, maana ikifika usiku utadai haki yako. Sasa hiyo haki yako atakupaje kama unavyohitaji maana amechoshwa na kazi ngumu za nyumbani.

Matatizo mengine sio husababishwa na shetani bali tuelewe kwamba na sisi ni binadamu, tunahitaji kuwa huru tunapofika umri fulani. Ukishakuwa mtu mzima na akili yako huwezi kuendeshwa kila kitu, kazini uendeshwe na boss wako, utukanwe mbele ya wafanyakazi wenzako. Urudi nyumbani nako utukanwe mbele ya mume wako na mawifi zako, kisa hukufanya kazi fulani.

Tuache utumwa, hakikisha mke wako yupo salama, anaweza akawa kimya asikuambie anavyojisikia. Ila elewa kwamba anatamani sana kurudi kwao, anatamani kurudi kwa ndugu zake, maana amechoka sasa.

Tafuta hata chumba kimoja cha kupanga, kama huna uwezo, wambie wazazi wako kama bado wanakupenda, wakupe nyumba nyingine ya kuishi nje ya hiyo mnayokaa pamoja na ukoo mzima.
Namaanisha kila mtu aliye wa hapo ana mamlaka ya kusema hii ni nyumba ya wazazi, naye anajihesabu yumo ndani ya miliki.

Ukiwa hujaoa bado, hakikisha unajipanga vizuri angalau uwe unaishi nje ya ndugu/wazazi wako. Sikufundishi kwamba mke wako asiwasaidie wazazi wako la hasha, iwe ni kwa sababu maalum. Labda wazee wanaumwa na hawana msaidizi wa kuwatunza na wamekuwa wazee sana hiyo haina shida, lakini ndoa yako iwe na heshima kwa watu wote, ikiwemo na ndugu zako.

Upendo una mipaka yake, sio kwa sababu umeona wazazi wanakupenda na unaona ukiwa mbali nao, utaonyesha chuki juu yao. Nakwambia utakuwa umetafsiri vibaya upendo, hebu jiulize kama mke wako angeonyesha upendo kwa wazazi wake angekubali kuondoka kwao na kuambatana nawe?

Au mke wako awe kila siku yupo kwao kama ni karibu, ama kama ni mbali iwe kila wikiend anakuomba pesa za kusafiri kidogo kwenda kuwasalimia wazazi wake, ungejisikiaje? jibu ni vibaya, sasa mwenzako naye anajisikia vibaya.

Mpaka hapo naamini umenielewa, ukiona ni upuuzi utakuwa unaitengenezea tanuru la moto, ndoa yako mwenyewe. Na mimi sipendi ikutokee hiyo, msikilize mke wako, hata kama unahisi hana point za kukuambia. Elewa kwamba hata yule unayemwona ni kichaa kuna muda anaweza akakufaa kabisa.

Rafiki yako Samson Ernest.
Wasiliana nami 0759808081.

Endelea kutembelea mtandao huu wa MTAZAMO WA MAISHA ili uendelee kubadili mawazo yako hasi na kuwa chanya.

SHARE

Samson Ernest

Habari, mimi ni mwandishi na mhamasishaji ambaye ninapenda kuona maisha ya kila mtu yakiwa bora. Naamini kila mmoja wetu anaweza kuwa na maisha mazuri kama ataamua hivyo. Karibu ujifunze kupitia mtandao huu wa MTAZAMO WA MAISHA.

  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

Post a Comment