Kukwama kwako, na kujiona kwako hauwezi tena kumechangiwa na nini? yaweza kuwa kumechangiwa na makosa ya nyuma? twende pamoja;
Unaposikia mtu amebadili historia ya maisha yake, kuna mawili, mwanzo alikuwa mtu mzuri na sasa amekuwa mtu mbaya kwa matendo yake, ama mwanzo alikuwa mtu mbaya kwa tabia zake na sasa yu mtu mzuri mwenye kuwafaa wengine.
Mara nyingi kuchoka na kujiona hufai huja pale unapokukumbuka matukio mabaya ya nyuma, na vilevile kuchoka huja pale unapokukumbuka ulivyokuwa vizuri hapo nyuma na sasa haupo vile ulivyokuwa.
Hizi nyakati mbili hupoteza dira za wengi wetu, wengi tumeshindwa kuchukua hatua ya kujenga maisha yetu upya kwa sababu ya maumivu ya nyuma.
Wengi tumeshindwa kuinuka tena kwa kuhesabu makosa tuliyotenda/tuliyotendewa, wengi wameshindwa kufanya vitu vya kuendelea kuonyesha thamani ya utu wao kwa makosa ya nyuma.
Akili yako inapoendelea kuwaza sana makosa, na inapoendelea kuwaza sana mafanikio ya nyuma kabla ya kuanguka, utainyima akili uhuru wa kufikiri makubwa zaidi ya sasa na ya mbele.
Kosa la nyuma, kwa mwanafanikio, hilo ni darasa lake la kufikia mafanikio makubwa. Naamini wewe unayesoma ujumbe huu ni mtu unayetafuta maarifa sahihi ya kukufikisha unapotaka na unaelewa ya nyuma hayawezi kuwa kitanzi kwako.
Kuanzia leo yale mawazo ya nyuma yaliyokufanya usisonge mbele, yaambie kwa heri, vinginevyo utajiua mapema sana na msongo wa mawazo.
Kufa mapema ni hasara kwa dunia, kwa sababu hujatimiza wajibu wako hapa duniani kwa kukata tamaa mapema, na hilo jukumu ulilolibeba ndani yako, ni lako na si la mwingine. Kama mwaka jana uliingia hasara kubwa kwenye biashara yako, ukaamua kuachana na biashara, nakushauri urudi haraka sana ukiwa na somo la kutorudia uzembe uliokupelekea kuingia hasara.
Na kama mwaka jana ulipanga uwe mwaka wako wa kufunga ndoa, lakini mambo yakaharibika njiani, usiache wazo hilo zaidi angalia njia nyingine na si kuleta chuki kwa kuona watu wote ni wale wale.
Na kama mahusiano yako ya ndoa yalivurigika, kaa chini ujue unaanzia wapi kuyarudisha tena, kama haiwezekani endelea mbele, maana Mungu bado anakupenda.
Waliobadilisha historia mbaya ya maisha yao ni wale waliokataa kunyanyaswa na ya nyuma, na walioandikwa kwenye vitabu vya dini/historia ni wale waliofanya mambo ya makubwa baada ya kuonekana nyuma walikwama.
Nakutakia leo yako ya mafanikio makubwa, kumbuka nyuma si kitanzi kwako, bali nyuma yako ni funzo kwako la kufanya vizuri leo.
Rafiki yako;
Samson Ernest.
+255759808081.
0 maoni:
Post a Comment